ujasiriamali February 2016 - UJASIRIAMALI
UJASIRIAMALI

UFUGAJI WA SAMAKI

03:15

Tasnia ya ufugaji wa samaki inajumuisha ukuzaji wa viumbe vya kwenye maji (bahari na maji baridi) katika mazingira tofauti na yale ya asili. Lengo kuu ni kukuza kwa muda mfupi ili kujipatia lishe, kipato na kutunza mazingira ya bahari, mito, maziwa nk.
Ufugaji unagusa viumbe vya kwenye maji kuanzia mimea kama vile mwani, samaki wasio na mapezi (kaa-crabs, kambamiti-prawns, chaza-oyster, majongoo bahari nk) na samaki wenye mapezi (perege/sato, kambale, kibua, trout, chewa nk).

Aina ya ufugaji

Zifuatazo ni aina/level za ufugaji ambazo mkulima anaweza kufanya kulingana na malengo na uwezo wake:

1. Huria (Extensive farming)

Idadi ya samaki wanaopandikizwa: samaki 2-3 kwa mita ya mraba
•Samaki hutegemea chakula cha asili (mimea ya majini-phytoplankton, wadudu/viumbe vidogo vya majini-zooplankton), Hauitaji ubadilishaji wa maji, Hauihitaji huduma ya ziada ya hewa

2. Kati ya huria na nusu shadidi (Modified extensive)  Idadi ya samaki, 4-7 kwa mita ya mraba

• Chakula cha asili na chakula cha ziada huitajika
• Maji hubadilishwa sentimenta 10-20 kila baada ya 3-4weeks kulingana na hali ya samaki na maji yako
• Huduma ya hewa ya ziada sio ya ulazima

3. Nusu shadidi (Semi-intensive)

• Idadi ya samaki kwa mita ya mraba ni 10-25
• Chakula cha asili na cha ziada
• Huduma ya hewa ya ziada lazima
• Maji hubadilishwa kila siku au kila baada ya siku kadhaa (15-25 cm)

4. Shadidi (Intensive)

• Idadi ya samaki ni zaidi ya 25 kwa mita ya mraba
• 100% chakula cha kutengenezwa
• Maji ni kuingia na kutoka
• Hewa ya ziada masaa yote
• Eneo linalotumika ni dogo ukilinganisha na mifumo mingine

Miundombinu ya ufugaji

Samaki wanaweza kufugwa katika miundombinu mbalimbali kama ifuatayo:

Bwawa
• Kina 0.8-1.5m
• Ukubwa 100 mita za mraba- 1ha

• Matanki

Umbo-mstatili au mviringo nk
Kina 1-1.5m
Kipenyo kwa lile la mduara 3-10m
Ukubwa kwa la mstatili inategemea na uwezo lakini lisiwe kubwa ili kuhimili nguvu ya maji
Materials: Plastic, cement, chuma nk
NB: Simtank linafaa( Faida inapatikana kama utalitumia kwa intensive system)

Vizimba (Fish cages)

Huwekwa katika maji ya asili kama vile ziwani, baharini au katika bwawa. Vipo vinavyoundwa kwa local materials kama mianzi na vipo vya aluminium.

Eneo linalofaa kwa ufugaji

Baadhi ya maeneo yanayofaa ni yale mashamba ya mpunga, na maeneo yaliyo karibu na vyanzo vya maji. Zifuatazo ni sifa za maeneo yanayofaa:

1. Udongo: Mfinyanzi husaidia kupunguza gharama za ujenzi wa bwawa na maji kwakuwa linaweza kutuamisha maji na kuruhusu maji yasipotee. Likiwa la kichanga bwawa ni lazima lijengewe au kuwekwa nylon sheet ili kuzuia upotevu wa maji. Unaweza ukahamisha udongo wa mfinyanzi kutoka sehemu moja hadi nyingine ili kuzuia upotevu wa maji (muone mtaalamu kwa ushauri zaidi juu ya mbinu ya kuhamisha udongo).

2. Chanzo cha maji ya uhakika
Eneo liwe na maji ya uhakika. Vyanzo vya maji ni kama vile mito, bahai, maziwa, chem chem., kisima, maji ya dawasco na mvua. Maji yasiwe na kemikali hatarishi kwa viumbe.

3. Miundombinu ya barabara: Inasaidia kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa na samaki wakati wa kuvuna.
4. Eneo lisiwe na historia ya mafuriko ili kuzuia athari za mafuriko kwa miundombinu yako. Utatumia gharama nyingi katika kuimarisha miundombinu yako.Jamii/aina ya samaki
5. Eneo lenye mwinuko wa wastani husaidia katika ujenzi wa bwawa.
6. Miundombinu ya umeme ni sifa ya ziada hususan kwa mkulima wa kati na wajuu kwa ajili ya kutumika katika kuendesha visambaza hewa.
7. Ulinzi muhimu

Note: Aina ya eneo lako ndilo linaweza kukufanya uchague muundombinu gani wa kufugia utumie

Aina ya samaki unaoweza kufuga Tanzania kwa sasa

Maji baridi

Sato/perege, Kambale, Kambamiti wa maji baridi na Trout (maeneo ya baridi kama vile Iringa, Kilimanjaro Arusha na Mbeya) na samaki wa mapambo.

Maji bahari

Kambamiti wa maji bahari, mwatiko, chewa, kaa, chaza wa lulu

Upatikanaji wa Vifaranga vya samaki husika

Vyanzo vya vifaranga ni kutoka katika mito, bahari, maziwa na wale wa kuzalishwa katika vituo vya kuzalishia vifaranga.

Sato na Kambale

Vituo vya serikali Utapata sato wa kike na kiume mixed sex). Kingolwira –Morogoro, LuhiraSongea, Mbegani-Bagamoyo . Kifaranga huuzwa Tsh. 50-100 kwa kifaranga.
Vituo binafsi kama vile Faith aquaculture-Kibamba (DSM) (utapata monosex sato), PeramihoSongea (mixed sex). Monosex huuzwa Tsh. kwa kifaranga, na mixed ni 100 kwa kifaranga.
Trout
Mayai huagizwa toka Marekani, Israel
Kambamiti wa baharini Alphakrust –Mafia.

Chakula cha samaki

Chakula cha asili

Hurutubishwa kwa mbolea ya wanyama kama vile kuku, ngombe, mbuzi nk. Kwa kiwango cha 1000kg/ha. Mbolea ya kuku ni kali hivyo unaweza punguza ikawa 250-500kg/ha.

Chakula cha kutengeneza

Samaki huitaji protein ili akuwe na kila samaki ana mahitaji yake hivyo ni species specific. Formula zipo kwa wale wanaotaka kutengeneza. Tanzania hakuna kiwanda kinachotengeneza. Ingredients zake ni kama vile dagaa, pumba, soya, unga wa ngano, unga wa muhongo nk.

Uvunaji

Kwa kawaida ni miezi 4-6 amabapo unapata 250-400g kulingana na ulishaji wako. Kwa prawns ni miezi 3-6 wanafikia 30-50g ambayo ni ukubwa wa soko.

Tathmini ya uchumi

Perege/sato Mfano:

Ukubwa wa bwawa ni 20m by 30m= 600 mita za mraba
Idadi ya samaki (7 kwa mita ya mraba) kwa monosex tu= 600 x 7=4200 fish
Uzito hadi kuvuna (4-6months)- 250g= 4200 x 250g= 1050kg (Nimesha convert gram to kg) Bei kwa kilo ni 6000-8000 kulingana na mahali= 6milion-8milion.

Gharama unazoweza kutumia

Ujenzi wa bwawa
Kuchimba kwa vibarua ni 500,000-600,000
Kuchimba kwa machine ni 1,000,000-1,500,000 kulinganana mahali ulipo

Kama udongo ni kichanga itabidi ujengee (kujengea ni gharama na inaweza ikafika 3.5-4m kwa gharama zote kuanzia kuchimba hadi kujengea).

Chakula cha kutengeneza tani 1 inaweza kugharimu laki 7-9. Hapa ili uweze kuzalisha tani 1 ya samaki aina ya perege utahitaji tani 1-1.5 ya chakula.
Gharama ya vibarua 150,000-250,000 kwa mwezi.
Utakuwa na gharama ya chokaa kwa ajili ya kuua vidudu (laki 100,000-200,000), mbolea kuzalisha chakula cha asili (gharama ni 50,000).

Jinsi ya kuhudumia bwawa, kuandaa chakula nitaandaa tips zingine.

UJASIRIAMALI

KANUNI ZA UFUGAJI BORA WA MBUZI NA KONDOO

10:39

Mbuzi na kondoo wanaweza kufugwa kwa gharama nafuu na kuishi katika mazingira magumu kama ya maradhi na ukame ikilinganishwa na ng’ombe. Kutokana na umbile lao dogo wanaweza kufugwa katika eneo dogo na pia wanaweza kuhudumiwa na familia yenye nguvukazi na kipato kidogo. Uzao wa muda mfupi unamwezesha mfugaji kupata mbuzi/kondoo wengi kwa kipindi kifupi.
Wanyama hao hufugwa kwa ajili ya nyama, maziwa, ngozi, sufu na mazao mengine kwa matumizi ya familia na kuongeza kipato.
 Ufugaji bora wa mbuzi na kondoo uzingatie kanuni zifuatazo:-
i) Wafugwe kwenye banda au zizi bora,
ii) Wachaguliwe kutokana na sifa za koo/aina na lengo la uzalishaji (nyama, maziwa au sufu),
iii) Wapatiwe lishe sahihi kulingana na umri na mahitaji ya mwili,
iv) Kuzingatia mbinu za kudhibiti magonjwa kama inavyoshauriwa na mtaalam wa mifugo,
v) Kuweka na kutunza kumbukumbu sahihi za uzalishaji; na
vi) Kuzalisha nyama, maziwa au sufu yenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko


Zizi au Banda la Mbuzi/Kondoo
Mbuzi/kondoo wanaweza kufugwa katika mifumo ya huria, shadidi na kwa kutumia njia zote mbili. Zizi hutumika katika mfumo huria ambapo mbuzi/kondoo huchungwa wakati wa mchana na kurejeshwa zizini wakati wa usiku. Zizi bora ni lile lenye sifa zifuatazo:-


• Lililo imara linaloweza kumkinga mbuzi/kondoo dhidi ya wanyama hatari na wezi,
• Lililojengwa mahali pa mwinuko pasiporuhusu maji kutuama,
• Ukubwa wa zizi uzingatie idadi na umri wa mifugo. Ni vema mbuzi/kondoo watengwe kulingana na umri wao; na
• Liruhusu usafi kufanyika kwa urahisi.
Pale ambapo mbuzi/kondoo wanafugwa kwa mfumo wa shadidi hufugwa katika
banda wakati wote. Banda bora la mbuzi/kondoo linatakiwa kuwa na sifa
zifuatazo:-
• Imara, lenye uwezo wa kuwahifadhi kiafya na pia dhidi ya hali ya hewa
hatarishi kwa mfano jua kali, upepo, baridi na mvua pamoja na wanyama
hatari,
• Lenye mwanga, hewa na nafasi ya kutosha inayoruhusu usafi kufanyika
kwa urahisi,
• Lijengwe sehemu isiyoruhusu maji kutuama na liwe mbali kidogo na
nyumba ya kuishi watu. Pia ujenzi uzingatie mwelekeo wa upepo ili hewa
kutoka bandani isiende kwenye makazi,
• Liwe na sakafu ya kichanja chenye urefu wa mita 1 kutoka ardhini (Kwa
banda la mbuzi),
• Liwe na sehemu ya kuwekea chakula, maji na mahali pa kuweka jiwe la
chumvichumvi; na
• Liwe na vyumba tofauti kwa ajili ya majike na vitoto, mbuzi/kondoo wanaokua, wanaonenepeshwa na wanaougua.
Vifaa vya Kujengea na Vipimo vya Banda
Inashauriwa banda la mbuzi/kondoo lijengwe kwa kutumia vifaa vinavyopatikana
kwa urahisi katika eneo husika. Ukubwa wa banda utategemea idadi yabuzi/kondoo wanaofugwa humo na ukubwa wa umbo
• Paa lijengwe kwa kutumia vifaa kama miti, mbao, na kuezekwa kwa nyasi,
makuti, majani ya migomba, mabati au hata vigae kwa kutegemea uwezo
wa mfugaji,
• Kuta zijengwe kwa kutumia mabanzi, mbao, nguzo, wavu wa waya, fito na
matofali. Kuta ziwe imara zinazoruhusu hewa na mwanga wa kutosha.
Mlango uwe na ukubwa wa sentimita 60 x 150,
• Sakafu inaweza kuwa ya udongo au zege. Sakafu ya kichanja inaweza
kujengwa kwa kutumia miti, fito, mianzi, mbao au mabanzi na iweze
kuruhusu kinyesi na mkojo kupita. Chumba cha majike na vitoto kiwe na
nafasi ya sentimita 1.25 kati ya papi na papi, fito na fito au mti hadi mti.
Chumba cha mbuzi/kondoo wakubwa iwe sentimita 1.9 kati ya mbao na
mbao.
Uchaguzi wa Mbuzi/Kondoo wa Kufuga
Madhumuni ya kuchagua mbuzi au kondoo wa kufuga ni kuboresha uzalishaji na
kuendeleza kizazi bora. Kuna aina nyingi za mbuzi/kondoo wanaoweza kufugwa
kulingana na mazingira na mahitaji ya mfugaji. Uchaguzi hufanyika kwa kuangalia
umbile, uzalishaji na kumbukumbu za wazazi kama vile umbo kubwa, ukuaji wa
haraka, uwezo wa kutunza vitoto na kutoa maziwa mengi.
Mbuzi wanaofaa kwa ajili ya maziwa ni aina ya Saanen, Norwegian na Toggenburg pamoja na chotara wao.
Mbuzi wanaofaa kwa ajili ya nyama ni Boer na chotara wao, mbuzi wa asili kama
vile Pare white, Newala na Ujiji. Mbuzi aina ya Malya (Blended) wanafaa kwa ajili
ya nyama na maziwa.

Aidha, kondoo aina ya Black Head Persian (BHP), Masai red, Suffolk na Hampshire wanafaa kufugwa kwa ajili ya nyama. Merino na Lincoln hufugwa kwa ajili ya sufu, wakati Corriedale na Romney hufugwa kwa ajili ya nyama na sufu. Hapa Tanzania kondoo wanaopatikana kwa wingi ni Black Head Persian, Masai Red Dopper na kondoo wengine wa asili.
Mbuzi/kondoo jike wanaofaa kwa ajili ya kuzalisha maziwa na nyama wawe na sifa
zifuatazo:-

• Historia ya kukua upesi, kuzaa (ikiwezekana mapacha) na kutunza vitoto
vizuri,
• Umbo la mstatili linaloashiria utoaji wa nyama nyingi; na
• Asiwe na ulemavu wa aina yoyote
Sifa za Ziada kwa Mbuzi wa Maziwa
• Awe na miguu ya nyuma iliyo imara na iliyonyooka na yenye nafasi kwa ajili ya kiwele; na
• Awe na kiwele kikubwa na chuchu ndefu zilizokaa vizuri
Sifa za Dume
Dume bora awe na sifa zifuatazo:-
• Miguu iliyonyooka, imara na yenye nguvu,
• Asiwe na ulemavu wa aina yoyote,
• Mwenye uwezo na nguvu ya kupanda; na
• Mwenye kokwa mbili zilizo kaa vizuri na zinazolingana
Angalizo: Dume lichaguliwe kwa makini kwa sababu “dume ni nusu ya kundi”.
Utunzaji wa Vitoto vya Mbuzi/Kondooa
Utunzaji huanza mara tu baada ya kuzaliwa.
Mfugaji ahakikishe:-
• Kitoto cha mbuzi/kondoo kinapata maziwa ya mwanzo (dang’a) ndani ya
masaa 24 tangu kuzaliwa na kwa muda wa siku 3,
• Kama kinanyweshwa maziwa, kipewe lita 0.7- 0.9 kwa siku. Maziwa haya, ni
muhimu kwani yana viinilishe na kinga dhidi ya magonjwa,
• Iwapo mama hatoi maziwa au amekufa, inashauriwa kutengeneza dang’a
mbadala au kama kuna mbuzi/kondoo mwingine aliyezaa anaweza kusaidia
kukinyonyesha kitoto hicho,
• Kitoto cha mbuzi/kondoo kiendelee kunyonya kwa wiki 12 - 16. Wiki 2 baada
ya kuzaliwa, pamoja na maziwa, kianze kupewa vyakula vingine kama nyasi
laini na chakula cha ziada ili kusaidia kukua kwa tumbo. Aidha, kipewe maji
wakati wote,
• Vyombo vinavyotumika kulishia vinakuwa safi muda wote,
• Kitoto cha mbuzi/kondoo kiachishwe kunyonya kikiwa na umri wa miezi 3 hadi
4 kutegemea afya yake; na
• Vitoto vipatiwe kinga na tiba ya magonjwa kulingana na ushauri wa mtaalam wa mifugo.
Matunzo Mengine
Utambuzi
Mbuzi huwekewa alama ili atambulike kwa urahisi na kuwezesha utunzaji wa kumbukumbu zake. Shughuli hii hufanyika kwa mbuzi/kondoo akiwa na umri wa
siku 3 - 14. Njia zitumikazo ni pamoja na:
• Kuweka alama sikioni kwa kukata sehemu ndogo ya sikio,
• Kumpa jina kwa wafugaji wenye mbuzi wachache,
• Kumvisha hereni ya chuma au plastiki yenye namba kwenye sikio,
• Kumvalisha mkanda wenye namba shingoni; na Kuweka namba kwa kuunguza sehemu ya ngozi ya mbuzi. Pale mfugaji anapotumia njia hii inashauriwa aweke alama kwenye eneo ambalo halitaathiri ubora wa ngozi
Kuondoa vishina vya pembe
Mbuzi/kondoo aondolewe vishina vya pembe akiwa na umri kati ya siku 3 hadi 14.
Visipoondelewa hukua na kusababisha kuumizana na kuhitaji nafasi kubwa
kwenye banda. Kazi hii ifanywe na mtaalam wa mifugo.
Kuhasi
Vitoto vya mbuzi/kondoo ambavyo havitatumika kwa ajili ya kuendeleza kizazi
vihasiwe kabla ya kufikia umri wa miezi 3. Kazi hii ifanywe na mtaalam wa mifugo.
Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo wa Miezi 4 - 8
Mbuzi wa miezi 4 mpaka 8 ni wale ambao wameacha kunyonya mpaka umri wa
kupandishwa kwa mara ya kwanza. Mbuzi wa umri huu wana uwezo wa kula aina
mbalimbali za malisho kama nyasi, mikunde, miti malisho na mabaki ya mazao
wakati kondoo hupendelea zaidi nyasi fupi. Wakati wa kiangazi huhitaji kupatiwa
chakula cha ziada au kupewa pumba za nafaka mbalimbali, mashudu ya alizeti,
pamba na dengu, majani ya mikunde yaliyokaushwa, madini na vitamini.
Katika ufugaji huria ni vema kuzingatia idadi ya mbuzi/kondoo inayoweza
kuchungwa katika eneo, aina na hali ya malisho.
Ili mbuzi/kondoo aweze kukua na kufikia uzito wa kuchinjwa/kupevuka mapema,
mfugaji anapaswa kufuata kanuni za ufugaji bora zifuatazo:-
• Kumpatia vyakula vya ziada kwa muda wa miezi 2 mfululizo kiasi cha kilo 0.2 –
0.7 kwa siku kuanzia anapoachishwa kunyonya,
• Kumpatia dawa ya kuzuia minyoo kila baada ya miezi 3 na kutoa kinga za
magonjwa mengine kama itakavyoshauriwa na mtaalam wa mifugo, Kuchanja na kuogesha ili kuzuia magonjwa mbalimbali,
• Kukata kwato mara zinapokuwa ndefu; na
• Kuhasi madume yasiyotumika kuzalisha.
Umri wa Kupandisha Mbuzi/Kondoo
Mbuzi/kondoo wakitunzwa vizuri wanaweza kupandishwa wakiwa na umri wa miezi 8 hadi 12 kwa mbuzi/kondoo walioboreshwa na miezi 18 hadi 24 kwa mbuzi wa asili kutegemea afya yake. Hata hivyo, inashauriwa wapandishwe wanapofikia uzito wa kilo 12 au zaidi na wasipandishwe mbuzi/kondoo wa ukoo mmoja.
Dalili za joto
Mfugaji anashauriwa asimpandishe jike kabla hajafikisha umri wa kupandwa wa miezi 8 hadi 12 kwa mbuzi/kondoo walioboreshwa na miezi 18 hadi 24 kwa mbuzi
wa asili hata kama ataonyesha dalili ya kuhitaji dume. Mbuzi/kondoo aliyezaa anaweza kupandishwa siku 30-60 baada ya kuzaa. Mbuzi/kondoo aliyeko kwenye
joto huonyesha dalili zifuatazo:-
• Hutingisha/huchezesha mkia,
• Hupanda na kukubali kupandwa na wengine,
• Hutoa ute mweupe ukeni,
• Huhangaika mara kwa mara na kupiga kelele,
• Hufuata madume,
• Hamu ya kula hupungua,
• Hukojoa mara kwa mara,
• Uke huvimba na huwa mwekundu kuliko ilivyo kawaida; na
• Kwa mbuzi anayekamuliwa hupunguza kiwango cha maziwa


Mbuzi/kondoo apelekwe kwa dume mara tu dalili za joto zinapoonekana kwani
joto hudumu kwa wastani wa siku 2 (saa 48). Chunguza tena dalili za joto baada
ya siku 19 hadi 21 na kama dalili hazitaonekana tena kuna uwezekano mkubwakuwa mbuzi/kondoo amepata mimba. Mfugaji apange msimu mzuri wa
mbuzi/kondoo kuzaa. Msimu mzuri ni mara baada ya mvua.
Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo Mwenye Mimba
Kwa kawaida mbuzi/kondoo hubeba mimba kwa muda wa miezi 5. Utunzaji wa
mbuzi/kondoo mwenye mimba ni muhimu kwani ndiyo chanzo cha kupata vitoto
vyenye afya bora. Mfugaji anashauriwa kufuata kanuni zifuatazo:
• Apatiwe vyakula vya ziada kilo 0.2 – 0.7 kwa siku ili kutosheleza mahitaji yake na kitoto kinachokua tumboni,
• Apatiwe nyasi, miti malisho na mikunde mchanganyiko kilo 1.8 – 2.5 kwa siku.
Dalili za Mbuzi/Kondoo Anayekaribia Kuzaa
• Huhangaika kwa kulala na kuamka mara kwa mara,
• Sehemu ya nje ya uke hulegea,
• Hujitenga na kundi na hutafuta sehemu kavu na yenye kivuli,
• Hupiga kelele; na
• Hutokwa na ute mzito ukeni.
Mfugaji akiona dalili hizi anashauriwa asimruhusu mbuzi/kondoo kwenda machungani, bali amtenge kwenye chumba maalum, ampatie maji ya kutosha na
kumuandalia sehemu ya kuzalia.

Utunzaji wa Mbuzi/Kondoo Anayenyonyesha
Mbuzi/kondoo anayenyonyesha huhitaji chakula kingi zaidi ili kukidhi mahitaji ya
mwili na kuzalisha maziwa kwa ajili ya kitoto/vitoto. Pamoja na nyasi, mikunde na
majani ya miti malisho kilo 1.8 – 2.5 kwa siku ni muhimu apewe chakula cha
nyongeza kilo 0.3 – 0.8 kwa kila lita ya maziwa inayoongezeka baada ya lita 2 na
maji safi, salama na ya kutosha wakati wote.

Taratibu za Kuzingatia Katika Ukamuaji wa Mbuzi wa Maziwa
Lengo la ufugaji wa mbuzi/kondoo wa maziwa ni kupata maziwa mengi, safi na
salama pamoja na mazao yatokanayo na maziwa. Mambo muhimu ya kuzingatia
ni:-
• Sehemu ya kukamulia iwe safi na yenye utulivu,
• Mbuzi/kondoo awe na afya nzuri, msafi, na kiwele kioshwe kwa maji safi ya
uvuguvugu,
• Mkamuaji asibadilishwe badilishwe awe msafi, mwenye kucha fupi na asiwe
na magonjwa ya kuambukiza,
• Vyombo vya kukamulia viwe safi; na
• Maziwa ya mwanzo kutoka kila chuchu yakamuliwe kwenye chombo maalum (strip cup) ili kuchunguza ugonjwa wa kiwele.
Utunzaji wa Dume Bora la Mbegu
Dume bora la mbegu ni muhimu litunzwe ili liwe na uwezo wa kutoa mbegu bora,
kupanda na kuzalisha. Dume bora huanza kupanda akiwa na umri kati ya miezi.8 -
10 kwa mbuzi walioboreshwa. Katika msimu wa kupandisha dume moja liruhusiwe
kupanda majike 40 hadi 50. Aidha, inashauriwa madume wenye umri wa miezi 8 –
9 waruhusiwe kupanda majike ambao ndio mara ya kwanza kupandwa.
Dume apatiwe:-
• Malisho ya kutosha na vyakula vya ziada kiasi kisichopungua kilo 0.2 – 0.7
kwa siku na maji ya kutosha,
• Majani ya miti malisho, mikunde na nyasi mchanganyiko na mabaki ya mazao; na
• Kilo 0.45 hadi 0.9 za chakula cha ziada za nyongeza kwa siku kulingana na uzito wake na wingi wa majike anayopanda.wiki 2 kabla na baada ya kuanza kupanda.

UJASIRIAMALI

NJIA NA UCHOCHORO WA KUEPUKNA NA UMASKINI IPO !!!!

06:07

KWANZIA LEO NDUGU MSOMAJI NTAKUWA NAKULETEA MAKALA MBALIMBALI KUHUSU NYIA MBALIMBALI ZA KUKIKWAMUA KIUCHUMI
MBINU, PAMOJA NA KAZI MBALIMBALI UNAZOWEZA KUZIFANYA ILI UONDOKANE NA UMASKINI NA MAWAZO POTOFU YA KUPENDA KUAJIRIWA

  • EMBU FIKIRIA UNAONAJE KAMA UTAKUWA UNAJIPANGIA MSHAHARA WAKO MWENYEWE 
  • UNAONAJE UKIJIITA BOS BADALA YA KUITA BOSI

Home

KILIMO CHA MATIKITI MAJI {WATER MELON}

05:06

Ili kulima matikiti maji inakubidi uwe na sehemu ya kutosha, yenye jua la kutosha, maji mengi na ardhi yenye rutuba ya kutosha, matikiti maji hukua haraka kama mimea mimgine ya jamii yake itambaayo mfano Matango, maboga na maskwash.
Kwa mtu ambaye anaanza kilimo yatampa tabu kidogo tofauti na Yule ambaye ana ujuzi kidogo na mambo ya kilimo kwa sababu yanahitaji umakini kiasi.

HALI YA HEWA

Mimea hii haihimili hali ya joto kali sana, mvua nyingi na udongo unaotuamisha maji, magonjwa ya fangasi na wadudu waharibifu, inastawi vizuri kwenye ukanda wa pwani na miinuko kidogo kama DSM,Tanga, Morogoro, Mtwara, lindi na Pwani ambapo kuna jua la kutosha. Muda mzuri wa kupanda ni kipindi cha kipupwe mwezi machi mpaka septemba .

UPANDAJI

Panda kwa kutumia Mbegu zinazouzwa madukani, ukitumia Mbegu kutoka kwenye tikiti ulilonunua linaweza likawa ni hybrid na matokeo yake matikiti yatakayozaliwa hayatakuwa bora kwa sababu yatakuwa ni kizazi cha pili 
Panda Mbegu yako moja kwa moja kwenye shamba, usinunue miche au kupanda Mbegu kwenye mifuko ya plastiki halafu ndo uhamishie shambani, panda Mbegu mbili sentimeta 2 chini ya udongo kwa umbali wa sentimeta 30 kutoka shina hadi shina na mita 2 - 3 kutoka mstari hadi mstari, baada ya siku chache Mbegu zitaanza kuota, baada ya kama wiki 2 katika Mbegu mbili ulizopanda kata moja na uache ule mche wenye afya zaidi, angalizo using’oe mche bali ukate ili kuzuia kusumbua mizizi ya mche uliobaki.
Unaweza kupandishia udongo kwenye mashina na hii itasaidia kupunguza maji yasituame kwenye mimea yako, pia unaweza kuweka samadi badala ya kupandishia udongo ukiwa na nia ileile ya kuzuia maji yasituame na kuongeza rutuba.
Kama una sehemu ndogo ya shamba unaweza kuyawekea matikiti waya wa kutambalia, ila inabidi uwe imara kwa sababu ya kuhimili uzito wa matunda yenyewe, na wakati wa kuanza kutambaa kwenye waya ni lazima uifundishe mimea kwa kuielekezea kwenye waya na kufungia

UANGALIZI

Miche ikiwa imetambaa kiasi unaweza kuweka matandazo kwenye udongo ili kuzuia upotevu wa unyevu, unaweza kuweka samadi au mbolea za viwandani, mimea ikiwa midogo tumia zaidi mbolea zenye nitrojen na utumie zaidi mbolea za potasiam mara baada ya maua kutokeza hadi matunda kukomaa, matawi yakifikia urefu wa mita 2 kata mbele ilikuruhusu kutoa matawi na hivyo kupata maua mengi zaidi hatimaye mavuno zaidi

MAUA NA MATUNDA

Matikiti hutoa maua dume na jike kwenye tawi moja, maua dume ambayo ni madogo zadi hutoka kwanza yakifuatiwa na maua jike ambayo ni makubwa zaidi, usipoona maua dume na jike kuna tatizo mfano maji kidogo yalimwagiliwa, upungufu wa viritubisho kwenye udongo, hali ya hewa ni joto/baridi sana n.k
Uchavushaji kwenye matikiti hufanyika na wadudu, kama huwaoni wakifanya kazi yao unaweza kufanya mwenyewe, muda mzuri ni wa asubuhi, unakata maua dume kwa kisu na kufanya uchavushaji kwenye maua jike, maua jike ya mwanzo kwenye tawi ndiyo yenye ukuaji bora zaidi, unaweza kukata tawi lisiendelee kukua baada ya matunda kutokeza hii husababisha kuwa na matunda makubwa zaidi

UVUNAJI MATIKITI

Ili kujua matikiti yamekomaa inahitaji ujuzi kidogo, upande wa chini wa tunda huanza kuwa na rangi ya njano, pia kikonyo juu ya tunda hukauka kabisa na kuwa kijivu, ila njia nzuri ni kuyapiga kwa kiganja na kusikiliza mlio wake kama tunavyofanya kwenye mafenesi, hii nayo ni shule nyingine. Tumia kisu wakati wa kuvuna matikiti, yabebwe na kuhifadhiwa vizuri kwenye makasha tayari kuuzwa au kwa matumizi binafsi

MAGONJWA NA WADUDU

Wadudu wa matikiti wako wanaoshambulia majani na maua, na wengine hushambulia matunda , pia kuna magonjwa ya fangasi ambayo hushambulia mimea, ili kujua dawa za magonjwa ni vizuri kuchukua sampuli na kwenda nayo kwenye duka la dawa na pembejeo za kilimo ili kupata dawa sahihi, dawa aina ya KARATE itasaidia kuua wadudu wa majani, maua na matunda na FUNGICIDE itasaidia kwa mashambulizi ya fangasi

Like us on Facebook

About me

Ismail mbaazi
Email: mbaazishumaa6@gmail.com
#+25565-9230-273