KILIMO CHA MATIKITI MAJI {WATER MELON}
05:06
Ili kulima matikiti maji inakubidi uwe na sehemu ya
kutosha, yenye jua la kutosha, maji mengi na ardhi yenye rutuba ya kutosha,
matikiti maji hukua haraka kama mimea mimgine ya jamii yake itambaayo mfano
Matango, maboga na maskwash.
Kwa mtu ambaye anaanza kilimo yatampa tabu kidogo
tofauti na Yule ambaye ana ujuzi kidogo na mambo ya kilimo kwa sababu
yanahitaji umakini kiasi.
HALI YA HEWA
Mimea hii haihimili hali ya joto kali sana, mvua nyingi
na udongo unaotuamisha maji, magonjwa ya fangasi na wadudu waharibifu, inastawi
vizuri kwenye ukanda wa pwani na miinuko kidogo kama DSM,Tanga, Morogoro,
Mtwara, lindi na Pwani ambapo kuna jua la kutosha. Muda mzuri wa kupanda ni
kipindi cha kipupwe mwezi machi mpaka septemba .
UPANDAJI
Panda kwa kutumia Mbegu zinazouzwa madukani, ukitumia
Mbegu kutoka kwenye tikiti ulilonunua linaweza likawa ni hybrid na matokeo yake
matikiti yatakayozaliwa hayatakuwa bora kwa sababu yatakuwa ni kizazi cha pili
Panda Mbegu yako moja kwa moja kwenye shamba, usinunue
miche au kupanda Mbegu kwenye mifuko ya plastiki halafu ndo uhamishie shambani,
panda Mbegu mbili sentimeta 2 chini ya udongo kwa umbali wa sentimeta 30 kutoka
shina hadi shina na mita 2 - 3 kutoka mstari hadi mstari, baada ya siku chache
Mbegu zitaanza kuota, baada ya kama wiki 2 katika Mbegu mbili ulizopanda kata
moja na uache ule mche wenye afya zaidi, angalizo using’oe mche bali ukate ili
kuzuia kusumbua mizizi ya mche uliobaki.
Unaweza kupandishia udongo kwenye mashina na hii
itasaidia kupunguza maji yasituame kwenye mimea yako, pia unaweza kuweka samadi
badala ya kupandishia udongo ukiwa na nia ileile ya kuzuia maji yasituame na
kuongeza rutuba.
Kama una sehemu ndogo ya shamba unaweza kuyawekea
matikiti waya wa kutambalia, ila inabidi uwe imara kwa sababu ya kuhimili uzito
wa matunda yenyewe, na wakati wa kuanza kutambaa kwenye waya ni lazima
uifundishe mimea kwa kuielekezea kwenye waya na kufungia
UANGALIZI
Miche ikiwa imetambaa kiasi unaweza kuweka matandazo
kwenye udongo ili kuzuia upotevu wa unyevu, unaweza kuweka samadi au mbolea za
viwandani, mimea ikiwa midogo tumia zaidi mbolea zenye nitrojen na utumie zaidi
mbolea za potasiam mara baada ya maua kutokeza hadi matunda kukomaa, matawi
yakifikia urefu wa mita 2 kata mbele ilikuruhusu kutoa matawi na hivyo kupata
maua mengi zaidi hatimaye mavuno zaidi
MAUA NA MATUNDA
Matikiti hutoa maua dume na jike kwenye tawi moja, maua
dume ambayo ni madogo zadi hutoka kwanza yakifuatiwa na maua jike ambayo ni
makubwa zaidi, usipoona maua dume na jike kuna tatizo mfano maji kidogo
yalimwagiliwa, upungufu wa viritubisho kwenye udongo, hali ya hewa ni
joto/baridi sana n.k
Uchavushaji kwenye matikiti hufanyika na wadudu, kama
huwaoni wakifanya kazi yao unaweza kufanya mwenyewe, muda mzuri ni wa asubuhi,
unakata maua dume kwa kisu na kufanya uchavushaji kwenye maua jike, maua jike
ya mwanzo kwenye tawi ndiyo yenye ukuaji bora zaidi, unaweza kukata tawi
lisiendelee kukua baada ya matunda kutokeza hii husababisha kuwa na matunda
makubwa zaidi
UVUNAJI MATIKITI
Ili kujua matikiti yamekomaa inahitaji ujuzi kidogo,
upande wa chini wa tunda huanza kuwa na rangi ya njano, pia kikonyo juu ya
tunda hukauka kabisa na kuwa kijivu, ila njia nzuri ni kuyapiga kwa kiganja na
kusikiliza mlio wake kama tunavyofanya kwenye mafenesi, hii nayo ni shule
nyingine. Tumia kisu wakati wa kuvuna matikiti, yabebwe na kuhifadhiwa vizuri
kwenye makasha tayari kuuzwa au kwa matumizi binafsi
MAGONJWA NA WADUDU
Wadudu wa matikiti wako wanaoshambulia majani na maua,
na wengine hushambulia matunda , pia kuna magonjwa ya fangasi ambayo
hushambulia mimea, ili kujua dawa za magonjwa ni vizuri kuchukua sampuli na
kwenda nayo kwenye duka la dawa na pembejeo za kilimo ili kupata dawa sahihi,
dawa aina ya KARATE itasaidia kuua wadudu wa majani, maua na matunda na
FUNGICIDE itasaidia kwa mashambulizi ya fangasi
0 comments