ujasiriamali January 2015 - UJASIRIAMALI
Home

Membe: Siwaonei wivu maswahiba wa mafisadi

15:48

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema hapendi ufisadi na anajua mafisadi hawampendi lakini, hawaonei wivu watu wanaopendwa na mafisadi.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 50 ya Dayosisi ya Dar es Salaam ya Kanisa la Anglikana Tanzania, ambayo alikuwa mgeni rasmi, Membe alitumia nafasi hiyo kuwataka waumini wa kanisa hilo kupambana na ufisadi katika ngazi zote nchini.

“Ninatosheka kupendwa na wale wenye mapenzi mema na Taifa letu. Sipendi rushwa na ufisadi. Ninashukuru Mungu kuwa rushwa, ufisadi na mafisadi hawanipendi zaidi,” alisema Membe.

Membe ambaye ni mbunge wa Mtama mkoani Lindi, alisema si jukumu la viongozi pekee au chama fulani pekee kupambana na ufisadi, bali ni wajibu wa kila mmoja kwa kuwa mafisadi wako katika ngazi zote.

“Ninaamini, mwaka huu, wengi wetu tukisema hivyo, tukasimama katika mstari huo na tukaenda hivyo, ufisadi hauwezi kutushinda. Kila mmoja asipuuze udogo wa sauti yake au uchache wetu dhidi ya wale waovu, maana hata mwale mdogo wa mshumaa hufukuza giza,” alisema Membe na kuongeza:

“Wako wanaotoboa mtumbwi wetu tunaosafiria pamoja na jitihada zetu za kupiga makasia.”

Kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, Membe ambaye pia anatajwa kuwania urais, alisema mwaka huu ni wa kipekee si tu kwa dayosisi hiyo inayoadhimisha miaka 50, bali pia kwa Watanzania wote: “Mwaka huu una mambo makubwa mawili yaliyo mbele yetu, yaani kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu.

“Uchaguzi wa mwaka huu ni muhimu kwani tunachagua rais mpya atakayeunda Serikali mpya ya awamu ya tano ambaye anatarajiwa kuendeleza mema ya awamu ya nne na awamu zilizopita na kutoa majawabu kwa changamoto za sasa na zijazo.”

Nchi majaribuni

Membe alisema nchi inapita katika majaribu na mitihani mikubwa kutokana na tatizo la mmomonyoko wa maadili katika ngazi zote kuanzia familia, shule, ofisini na serikalini.

“Tunalo tatizo la ufisadi, ukatili dhidi ya vikongwe na watu wenye ulemavu wa ngozi na tunalo pia tatizo la umaskini. Tunalo tatizo la kupoteza uvumilivu wa kidini na kisiasa.”
Aliongeza kuwa Watanzania wengi wamefika mahala wanaanza kukata tamaa na kupoteza matumaini: “Kimsingi, waumini wamekata tamaa na kupoteza hofu ya Mungu kiasi cha wengine kukimbilia kwenye nguvu za giza, uganga na unajimu. “Tunahitaji kutoka hapa. Tunajiuliza wote, tunatokaje”.

Aliliomba Kanisa na waumini waliombee Taifa ili Mungu awaongoze kuchagua viongozi wenye uwezo, busara na hekima ya kutatua changamoto zinazolikabili Taifa.

“Tuchague viongozi waadilifu, wazalendo, wachapa kazi, wasio na uchu wa madaraka kwa ajili ya kujinufaisha wao binafsi na marafiki zao.

“Ninawasihi viongozi wa dini muongeze juhudi za kuhubiri umoja na kutoa mafundisho ya kuhimiza udugu na mshikamano miongoni mwa waumini na Watanzania kwa jumla. Watu wapendane na washirikiane bila kujali itikadi za vyama vyao au ushabiki kwa wagombea. “Tukumbushane kuwa chaguzi zinakuja na kuondoka lakini amani yetu, usalama wetu, udugu wetu na umoja wetu ndiyo nguzo kuu za uwepo wa Taifa letu.

Askofu Mokiwa

Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa alisema ni wakati mwafaka kwa vijana kujitambua na kutokubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa kwa masilahi yao binafsi.

Dk Mokiwa alisema kuwa vijana wanatumiwa na wanasiasa kwa sababu wengi wao hawana ajira, hivyo wanasiasa hao wanatumia mwanya huo kuwarubuni ili kutimiza malengo yao kisiasa ambayo hayana faida kwao.


“Vijana ndiyo wenye hii nchi, hivyo ni wakati wenu kusimama imara ili Taifa hili lisonge mbele, pia msikubali kutumiwa na baadhi ya wanasiasa hasa wakati huu tunapoelekea kwenye uchaguzi mkuu,” alisema askofu huyo.

Alisema katika siku za karibuni vijana wamegeuka walinzi wa masilahi binafsi tofauti na ilivyokuwa miaka iliyopita ambayo walijitoa kwa ajili ya kutetea na kuilinda nchi.

Dk Mokiwa aliwataka wananchi wasikubali kugawanywa kwa misingi ya tofauti za kiitikadi hasa katika mchakato wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu.

“Tusikubali makundi haya yakavunja umoja wetu,” alisema Dk Mokiwa na kuongeza kuwa umoja ukitoweka hata hawa ‘panya road’ wataendelea kufanya maovu.

Like us on Facebook

About me

Ismail mbaazi
Email: mbaazishumaa6@gmail.com
#+25565-9230-273